Baadhi ya wakazi wa jimbo la Ruangwa mkoani Lindi wamediriki kusema kuwa sasa wamepata mbunge ambaye kwa muda mrefu walikuwa wakimhitaji awawakilishe bungeni.
Hii inatokana na makubwa ambayo mbunge wao, Kassim Majaliwa amekuwa akiyafanya kwa kipindi kifupi ambacho amechaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo.
Hili limeendelea kuonekana kwa jinsi ambavyo amekuwa akihangaika huku na huko ili kuhakikisha kwamba jimbo hilo linapata maendeleo katika nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu.
Hivi karibu mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI anayeshughulikia elimu alipokea vitabu 900 kwa ajili ya shule 20 za wilaya ya Ruangwa.
Vitabu hivyo vilitolewa na Maktaba Kuu ya Taifa na Mkurugenzi wake, Alli Mcharazo na kukabidhiwa kwa mheshimiwa Majaliwa ili akavigawe kwa shule 20 zikiwemo 10 za msingi na 10 za sekondari.
Mheshimiwa Majaliwa anatarajia kupeleka vitabu hivyo mwanzoni mwa mwezi Septemba mwaka huu wa 2011 ambapo pia mbunge huyo ana mpango wa kutoa jengo litakalotumika kama maktaba ya wilaya.
Kwa hatua hii na mengine mengi ambayo amekuwa akiyafanya kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa jimbo lake, baadhi ya wananchi wamesema kuwa huyo ndiye mbunge waliyekuwa wakimhitaji kuwa mwakilishi wao bungeni.
No comments:
Post a Comment