Monday, August 8, 2011

Hekima ya mbunge Kassim Majaliwa yawaokoa wakuu wa Idara za Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa

Wakuu wa idara mbalimbali za Halmshauri ya wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, walijikuta katika wakati mgumu kufuatia taarifa yao ya shughuli za maendeleo kukataliwa na wajumbe wa Halmshauri Kuu ya CCM ya wilaya hiyo.
Tukio hilo lilitokea Agosti 6, 2011 katika ukumbi wa jengo la Chama cha Walimu wilayani humo mara baada ya Afisa Mipango wa wilaa hiyo Godfrey Lwambano kusoma taarifa hiyo ndipo ukafika wakati wa kuijadili.
Kwenye majadiliano hayo ilibainika kuwa kilichosomwa na Afisa huyo haikuwa na ukweli wowote na hasa kuhusu miradi ya maendeleo, mikopo kwa vikundi mbalimbali wakiwemo wanawake na vijana na mambo mengine.
Hali hiyo ilisababisha kuzua maswali mengi magumu ambayo wakuu wa idara walikuwa na majibu mepesi na kusababisha malumbano makali hadi mbunge wa jimbo la Ruangwa Kassim Majaliwa alipoingia kati kuokoa jahazi.
Bila hekima ya mbunge huyo, wakuu hao wa idara walikuwa na wakati mgumu kujibu makombora yaliyoelekezwa kwao na wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM ambao walukuwa na kiu ya kutaka kupata ukweli kuhusu taarifa hiyo.
Baada ya kuona mambo yanakwenda ndivyo sivyo, mbunge huyo aliingilia kati na kuwaambia wakuu hao wa idara kuwa taarifa yao ilijaa maswali mengi kuliko majibu na kushauri kuwa ikaandaliwe upya.
Ushauri huo wa mbunge ulipokelewa kwa shangwe na wajumbe hao ambapo wakuu wa idara walilazimika kuondoka kwenye kikao hicho ambapo sasa taarifa  yao huenda ikajadiliwa mwezi Septemba.

No comments:

Post a Comment